Na Marko Gideon
Dar es Salaam, Oktoba 31 (IPS) – Afrika ina wastani wa wakazi milioni 991, lakini ni wastani wa wakazi milioni 66 tu ndio wanaotumia intaneti. Takwimu hizi, kwa mujibu wa mtandao wa World Internet Statistics, ni asilimia 3.9 tu ya watu wanaotumia intaneti duniani.
Bara la Asia linaongoza kwa kuwa na asilimia 42 na Ulaya inafuatia kwa kuwa na asilimia 24. Amerika Kaskazini ina asilimia 15 na Amerika Kusini asilimia 10.
Nchini Tanzania, ni asilimia 0.8 tu ya wananchi wanatumia intaneti, nyuma ikilinganishwa na nchi jirani za Kenya na Uganda. Wakati Kenya ni asilimia 5, Uganda ni asilimia 3.8.
Hii inajitokeza hata kama sera ya teknohama Tanzania inalenga katika kuifanya teknohama kuchangia katika maendeleo ya taifa na kujenga jamii yenye maarifa zaidi kwa kutumia teknohama.
Pamoja na matumizi ya itaneti kuonekana kuwa ya chini nchini, hata hivyo, bado teknolojia hiyo ni muhimu katika kufanikisha mambo mengi ya kimaendeleo.
Katika fani ya habari, intaneti ni muhimu katika shughuli za kila siku za waandishi wa habari.
Kulingana na Peik Johansson, mratibu wa shirika la Vikes nchini Finland, intaneti kwa waandishi wa habari inatumika zaidi katika mambo makuu manne – kuwasiliana, kufuatilia habari, kuchapisha habari na utafiti.
Mambo haya manne ni miongoni mwa mada katika mfululizo wa mafunzo ya intaneti yanayoendeshwa nchini kote na MISA-Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Mawasiliano na Maendeleo la Finland (VIKES).
Katika mafunzo ya karibuni yaliyofanyika kati ya tarehe 25–30 jijini Mwanza, ambayo yalileta washiriki kutoka mikoa ya kanda ya ziwa ya Kagera, Shinyanga, Mwanza na Mara, Peik alisema kwa sasa Tanzania ina zaidi ya vyombo vya habari 20 ambavyo vina tovuti zenye taarifa za mara kwa mara.
“Haya ni mabadiliko ya kasi katika muda mfupi,” anasema Peik katika tovuti yake. “Tangu mwaka 2006 kulikuwa na vyombo vya habari vitatu tu ambavyo vilikuwa na tovuti.”
Waandishi waliohudhuria mafunzo hayo walihisi mapinduzi katika fani yao. “Ni ndoto iliyotimia kwa waandishi wa habair wengi katika kanda ambapo ni wachache tu wanatembelea tovuti binafsi ukiachilia mbali kuwa na tovuti zao,” alisema Deus Bugaywa , mmoja wa washiriki kutoka Mwanza katika tovuti yake aliyoitengeneza wakati wa mafunzo hayo.
Akitoa maneno machache ya shukrani kwa niaba ya washiriki wengine kumshukuru mkufunzi wa mafunzo hayo wakati wa kuhitimisha, Bugaywa alisema “mafunzo haya yanafanya uandishi wetu kuwa wa kisasa.” Aliongeza “sasa tumekuwa wanamawasiliano wa kisasa na kisayansi.”
Kwa upande wa Victor Maleko, ambaye pia ni mshiriki kutoka Mwanza, “intaneti inaweza kuwa karibu kila kitu ambacho unakitafuta lakini unatakiwa kujua ni nini unakitafuta na ni nani anakupatia taarifa hiyo.”
Alisema mara nyingine siyo muhimu kujua nani anakupatia taarifa kwasababu kuna injini nyingi za kutafutia taarifa kama vile google.
“Kupitia intaneti unaweza kupata vyanzo vya taarifa au unaweza kupata mkusanyiko wa taarifa za kimataifa, pia unaweza kutafuta taarifa za kweli na habari za zamani na watu au hata kutumiwa na wahariri kuthibitisha ukweli wa habari,” anasema Maleko katika tovuti yake.
Siyo waandishi wa habari tu nchini Tanzania ambao wanafaidika na huduma ya intaneti. Pamoja na Tanzania kushika nafasi ya chini katika kuwa na watu wengi wanaotumia intaneti, matumizi yanaongezeka kwa kasi katika jamii. Likinukuu utafiti wa gazeti la Business Times, shirika la Balancing Act, linasema katika tovuti yake kuwa maelfu ya watu wanamiminika katika vibanda vinavyotoa huduma za intaneti, jijini Dar es Salaam na mahali pengine nchini. Taarifa hiyo inasema kwa sasa kuna vibanda vya huduma ya intaneti zaidi ya 20 katikati mwa Dar es Salaam pekee, na mjini Zanziabar, idadi inafika tano.
Pia ongezeko la watumiaji limekwenda sambamba na kupungua kwa gharama za kutumia intaneti, kulingana na Balanci Act, huku bei ikishuka kutoka wastani wa dola 1.25 hadi dola 0.625 kwa saa.
Watumiaji wakuu wa intaneti ni pamoja na wanafunzi, vijana, wafanyabiashara, wafanyakazi wa ofisini na wasomi.
Mabadiliko katika matumizi ya intaneti pia yanaonyeshwa katika World Internet Statistics, ambapo kati ya mwaka 2000–2009, idadi ya watumiaji wa intaneti imeongezeka kwa asilimia 352.2.
Tangu mwaka jana, MISA-Tazania kwa kushirikiana na VIKES kwa ufadhili wa serikali ya Finland wamekuwa wakilenga kutoa mafunzo ya intaneti kwa waandishi. Hadi sasa mafunzo yameshatolewa kwa takribani waandishi 80 nchini kote.
Lakini hata hivyo, mafanikio haya yanaweza kukabiliwa na vikwazo kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na lugha na upatikanaji wa nishati, hasa katika maeneo ya vijijini.
“Umeme ni tatizo katika maendeleo ya intaneti nchini,” alisema Robinson Wangaso, mshiriki mwingine katika mafunzo hayo kutoka Mara.
Hata hivyo, Wangaso anadhani kuna njia mbadala za kuondokana na kikwazo hicho. “Lakini mtu anaweza kutumia simu ya mkononi, au hata kompyuta ndogo ambayo anaweza kuichaji,” anasema. “Ni changamoto lakini kuna namna ya kuweza kuikabili.”